Simulizi : Kifo Siku Ya Harusi Yangu
Sehemu Ya Kwanza (1)
IMEANDIKWA NA : ERIC SHIGONGO
********************************************************************************
Simulizi : Kifo Siku Ya Harusi Yangu
Sehemu Ya Kwanza (1)
MWANZO
Mamia ya watu walikuwa wamefurika ndani ya ukumbi wa Pundamilia ulio ndani
ya hoteli ya maarufu ya Atrium, karibu kila mtu maarufu nchini Tanzania alikuwa
ndani ya ukumbi huu. Kuanzia Rais, Mawaziri, Makatibu Wakuu, wanamichezo,
wasanii na wafanyabiashara wakubwa wa Kiasia na Afrika. Hakika ilionekana siku
ya furaha, watu wakiwa wameketi kwenye meza zao wakiendelea kunywa
vinywaji taratibu.
Wanaume wakiwa wamevalia suti nyeusi na wanawake magauni ya rangi nyeupe
na zambarau, hakika walipendeza. Kila nilipozungusha macho yangu huku na kule
ndani ya ukumbi nilionekana kutoamini kilichokuwa kinatendeka, hatimaye
baada ya safari ndefu ya kupanda na kushuka milima, nilikuwa namuoa Bianca
Rwegoshora, mtoto wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Wazazi na ndugu wa pande zote mbili walionekana kufurahia kila kitu kilichokuwa
kikitokea ukumbini, kwao hakika ulikuwa ushindi, walikuwa wamefanikisha
kutokea kwa jambo ambalo kwa muda mrefu walilihangaikia sana, kuhakikisha
kwamba namuoa Bianca badala ya Farida Mbaraka, kisa tu alikuwa ni mtoto
aliyetokea familia duni, wazazi wake wakiwa hawana elimu hata ya darasa la saba.
Hicho ndicho kilikuwa kikwazo, hakuna aliyeuangalia uzuri wake, wala ukarimu
wa moyo wake, alihukumiwa sababu ya umasikini wake, hakika iliuma.
Asilimia kubwa ya ndugu zangu waliokuwa ukumbini, macho yangu
yalivyowapitia, sikumpata hata mmoja ambaye hakuwa na digrii! Wengi walikuwa
ni madaktari, maprofesa, wenye elimu ya chini kabisa walikuwa ni wenye digrii
moja pamoja na wanafunzi waliokuwa vyuoni na sekondari ambao pia
walitegemea kuingia kaburini wakiwa na digrii si chini ya tatu.
Hiyo ndiyo ilikuwa familia yangu, familia ya wasomi, walioheshimu watu kwa
alama zilizotangulia majina yao, mfano Dk., Injinia, Mchumi, Mwanasheria, n.k.
Mtu yeyote ambaye hakuwa na vitangulizi vya taaluma yake, hakuheshimiwa na
familia yangu. Hicho ndicho kilichompata Farida Mbaraka, kwa sababu ya familia
yake kutokuwa na elimu, alionekana kama kinyaa, ingawa nilimpenda mno, baadhi
ya ndugu zangu waliomo ukumbini wakishangilia, walimkashfu na kusema
kwamba kumuoa ingekuwa ni kutumia sheria iitwayo “The Dilution Law”.
“Mtoto huchukua akili kutoka kwa baba na mama, ukiwa na akili nyingi, halafu
ukaoa mwanamke au kuolewa na mwanaume asiyekuwa na akili, mtoto wako
atakuwa na akili kidogo, lakini ukioa mwanamke au kuolewa na mwanaume
mwenye akili nyingi, lazima watoto wako watakuwa vipanga sana darasani!” Hayo
yalikuwa ni maneno ya Joackim, mtoto wa baba yangu mkubwa ambaye yeye
katika umri wa miaka thelathini tu alikuwa anasomea digrii ya tatu nchini
Marekani. Alikuwepo ukumbini akishangilia juhudi zake za kuhakikisha simuoi
Farida bali Bianca, ambaye karibu familia yake yote ilikuwa ni ya wanasheria.
“Genesis!” Ilikuwa ni sauti ya Bianca akiniita, nikageuza kichwa changu
kumwangalia, ili kumfanya asigundue kwamba nilikuwa na mawazo, niliusogeza
mdomo wangu karibu na wake na kumbusu, wapiga picha wakafanya kazi yao.
“Yes sweetie!” (Ndio mpenzi)
“What is going on your mind?”( Nini kinaendelea kichwani mwako?)
“Why?”(Kwanini?)
“You seem to be contemplating too hard!”(Unaonekana kufikiria sana)
“No! I am just thinking about our future, where we have come from, where we are
and where we are going!”(Hapana! Nafikiria tu kuhusu maisha yetu ya baadaye,
tulikotoka, tulipo na tunakokwenda!)
“Isn’t Farida on your mind?”(Farida hayupo kichwani mwako?)
“Me? No way! That drug dealer? Probably she is dead by now.”(Mimi? Huyo muuza
madawa ya kulevya? Labda amekwishakufa tayari) niliongea nikichukua kitambaa
na kujifuta machoni.
Si kweli kwamba nilikuwa simpendi Farida, kila jina lake lilipotajwa huzuni
iliniingia na machozi kunilengalenga, nilimpenda sana msichana huyo na katika
maisha yangu sikuwahi hata mara moja kukutana na msichana wa aina yake.
Alikuwa na sifa zote, kuanzia uzuri wa sura na maumbile mpaka tabia na
mwenendo wake na hicho ndicho nilichohitaji kutoka kwa mwanamke wa kuishi
naye maisha, sifa ambazo wazazi na ndugu zangu katu hawakuziona, kwao kitu
cha muhimu kilikuwa ni elimu.
“Then why are you so sad? Are you not happy that we are finally married?”(Sasa
kwanini una huzuni siku ya harusi yetu? Haufurahii kwamba hatimaye
tumeoana?)
“I am so happy and excited, though I can’t stop myself thinking of Farida.”(Nina
furaha sana ingawa siwezi kujizuia kumfikiria Farida)
“But a few minutes ago you said she is not on your mind!”(Lakini dakika zilizopita
ulisema hayupo akilini mwako)
“Let me just be brutally honest with you! I can’t stop thinking of Farida.”(Acha tu
niwe muaminifu kupita kiasi, siwezi kuacha kumfikiria Farida) niliongea
nikimwangalia Bianca, akainamisha kichwa chake chini kuonyesha maelezo yangu
yalimwumiza, lakini ilikuwa ni bora aumie akiwa ameambiwa ukweli.
Haikuwa rahisi kumsahau Farida, kila siku alisumbua akili na mawazo yangu,
mpaka wakati huo nilikuwa sijaamini kabisa kwamba alikuwa ni mfanyabiashara
wa dawa za kulevya, aliyekamatwa na madawa hayo nchini Saudia Arabia siku
chache tu kabla ya kumvisha pete ya uchumba na kilichokuwa kikisubiriwa ni
kupigwa risasi mbele za kadamnasi, hiyo ndiyo ilikuwa adhabu ya watu
waliokamatwa na madawa hayo katika nchi za Uarabuni.
“Lakini aliondoka kwa lengo la kwenda kufanya usaili ili ajiunge na Chuo Kikuu
cha Riyadh, naye akitamani awe angalau na digrii na familia yangu iweze
kumkubali. Alifanya kila kilichowezekana ili wazazi wangu wampende. Hivi ni
kweli Farida alikuwa akifanya biashara ya madawa?” nilijiuliza bila kupata majibu.
Ingawa Bianca alikuwa kando yangu, tena siku ya harusi yetu bado kichwani
mwangu alikuwemo Farida, fikra za kwamba angekuwa amekwishapigwa risasi
mpaka wakati huo zilinisumbua sana kiasi cha kunifanya nisifurahie kitu chochote
kilichokuwa kikiendelea ukumbini ingawa karibu kila mtu alishangilia mimi na
Bianca kufunga ndoa. Nilichotaka kufanya wakati huo ni kuondoka ukumbini
kwenda chumbani kupumzika.
Ghafla nilisikia mlio wa ujumbe wa simu kwenye simu yangu, nikijua ni kutoka
kwa baadhi ya rafiki zangu waliokuwa wakinitumia ujumbe wa pongezi.
Nilinyoosha mkono na kuichukua simu yangu mezani, kisha kufungua sehemu ya
ujumbe na kuanza kusoma, moyo wangu ulishtuka nilipoona maneno “Siri kubwa”.
Nikazidi kusogea chini ambako kulikuwa na anuani ya barua pepe ya Bianca, pia
ikiwa na alama yake ya siri ya kufungulia kama kuna mtu alitaka kusoma. Chini
yake kukiwa na maandishi “Tumekuletea hii, ili uingie kwenye sanduku la barua
pepe la mkeo, ili upate kumwelewa vizuri na unyama aliomfanyia Farida.”
Moyo wangu ukaruka mapigo kadhaa, jasho likaanza kunitoka, huku nikihisi kama
vile shinikizo langu la damu lilikuwa likishuka kwa kasi. Sikutaka tena kukaa
ukumbini, ujumbe huo wa simu ndio ulichochea kabisa hamu yangu ya kuondoka
kwenda chumbani kupumzika ambako lengo langu lilikuwa ni kwenda moja kwa
moja kwenye kompyuta na kufungua anuani ya barua pepe ya Bianca na kujionea
kilichokuwemo ndani. Moyoni nilijawa na hofu, nikiogopa ambacho ningekikuta
lakini bado nilitamani kujua.
“Sijisikii vizuri!” nilimgeukia Bianca na kumweleza.
“Nini tena?”
“Nataka kwenda kupumzika, ni vizuri tukaondoka.”
“Genesis, tuondoke mapema kiasi hiki? Kabla wazazi hawajaondoka?”
“Naumwa!” nilitoa kisingizio huku nikigeuza kichwa kuongea na Kelvin, mpambe
wangu wa siku hiyo. Mimi na Kelvin tulisoma pamoja Chuo Kikuu cha St. Augustine
kilichopo mjini Mwanza, alikuwa rafiki yangu mkubwa na tulishirikiana mambo
mengi.
“Vipi tena?” aliniuliza.
“Aisee mwambie MC atangaze kuwa tunaondoka kwenda chumbani kupumzika.”
“Eti shemeji?” Kelvin alimuuliza Bianca.
“Kama yeye ameamua mimi sina kizuizi”
Bila kipingamizi Kelvin alifanya kama alivyoombwa, MC akatangaza juu ya
kuondoka kwetu na watu wote wakasimama huku wakishangilia, tukitembea kwa
madaha tukiwa tumeshikana mikono kuelekea nje ya ukumbi ambako tuliingia
kwenye lifti na kwenda moja kwa moja ghorofa ya tatu, kilipokuwa chumba chetu,
Kelvin na mke wake Martina walikuwa pamoja na sisi mpaka ndani ambako bila
kuchelewa walituaga na kuondoka.
Kitu cha kwanza nilichofanya ni kwenda kwenye kompyuta yenye mtandao wa
Internet, haraka nikaiwasha na kuingia kwenye tovuti ya G-mail nikaandika
Bianca10@Gmail.com, kisha kwenye alama ya siri nikaandika neno Hadohado,
hiyo ndiyo ilikuwa alama ya siri ya Bianca. Niliyafanya yote hayo akiwa amejilaza
kitandani, bila kunisogelea. Nikabonyeza sehemu iliyoandikwa Sign in, muda
mfupi tu baadaye sanduku lake la barua pepe likafunguka, iliyokuwa juu kabisa
iliandikwa “The truth about innocent Farida Mbaraka”
Maneno yaliyomaanisha ukweli kuhusu Farida Mbaraka asiye na hatia. Moyo
wangu ukapiga kwa kasi, jasho likinitoka huku nikisubiri ifunguke, sekunde
chache baadaye kila kitu kilikuwa wazi nikaanza kusoma huku nikibubujikwa na
machozi, mara kadhaa niligeuza shingo yangu kumwangalia Bianca aliyekuwa
amejilaza kitandani, hasira ikazidi kunipanda zaidi na zaidi, nilimwonea Farida
huruma kiasi cha kutamani kuua, hakustahili unyama aliotendewa kwa sababu
yangu. Sikumchukia Bianca peke yake bali pia familia yangu.
Hatimaye nikafikia uamuzi wa kufanya nilichoona kinafaa, kama Farida alikuwa
ameshapigwa risasi sababu ya madawa ya kulevya ambayo hakuyamiliki, basi
waliofanya mpango huo nao hawakustahili kuishi hata kama walikuwa ni ndugu
zangu na wa kwanza kufa alitakiwa kuwa Bianca! Nikanyanyuka nilipokuwa
nimeketi na kutembea mpaka kwenye meza iliyokuwa pembeni, juu yake
kulikuwa na sinia lenye chakula, pia vikiwepo visu na uma.
“Hiki kinatosha!” niliwaza wakati nakichukua kisu na kuanza kutembea taratibu
kuelekea kitandani alipolala Bianca akiwa hajui kilichoendelea, nikahesabu moja
mpaka tatu kisha kushusha mkono kwa kasi kifuani kwake upande wa moyo,
damu nyingi ikaruka na kulowanisha nguo zangu, nikakichomoa tena na
kukizamisha mara ya pili kisha kuchukua mto na kumgandamiza nao Bianca
mdomoni ili kelele zake zisitoke nje, dakika tano baadaye alitulia, tayari
alishakufa.
“Mungu wangu nimefanya nini? Kwanini nimeua? Si ningemwacha tu na kutafuta
mwanamke mwingine?” niliwaza nikimwangalia, ilikuwa kama vile niliachiwa na
shetani aliyekuwa amenifunika na kuuona ukweli wa ubaya nilioutenda.
Lakini kwanini nimeua siku ya harusi yangu? Nimesoma nini kwenye barua pepe
hii?
Ilionekana kuwa siku ya furaha kubwa, Genesis mtoto wa tajiri alikuwa akimuoa
binti mrembo aitwaye Bianca, mtoto wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Watu
wote maarufu walikuwa ndani ya ukumbi kushuhudia tukio hilo la kihistoria bila
kufahamu kuwa lingeishia kwenye mauaji, Genesis akiwa amemuua kwa
kumchoma kisu Bianca wakiwa chumbani, kisha yeye mwenyewe kujirusha
kupitia dirishani ili aanguke chini na kufa. Kwanini aliamua kufanya mauaji hayo
ya kikatili? Je, alipojirusha dirishani alikufa?
Genesis anasimulia historia ya maisha yake, jinsi alivyozaliwa kwenye familia ya
wasomi ambao hata siku moja hawakukubaliana na suala la mtoto wao kuoa au
kuolewa na mtu asiyekuwa msomi. Akiwa kidato cha pili katika shule ya kimataifa
ya Mtakatifu Thomas mkoani Morogoro, msichana mrembo aitwaye Farida
anahamia katika shule hiyo kutoka shule ya Sekondari ya Kilakala.
Kihistoria msichana huyu anatoka familia maskini sana, wazazi wake hawakupata
elimu hata kidogo. Pamoja na hayo, Farida alikuwa na akili nyingi kupita kiasi,
zilizomfanya ashike namba moja kwenye mtihani wa taifa Tanzania nzima. Tukio
hili ndiyo lilimfanya Padri Bathromayo wa Shirika la Kitume la Women Oppotunity
Expanded, aamue kumhamisha Farida kutoka Kilakala kwenda shule ya Sekondari
ya Mtakatifu Thomas, gharama zote za masomo yake zikichukuliwa na shirika hilo.
Baada ya kutambulishwa darasani, Farida akatokea kuwa rafiki mkubwa wa
Genesis pamoja na kijana mwingine aitwaye Chris. Katika mazungumzo yao,
Farida ambaye ameitingisha shule hiyo kwa uzuri wake, wavulana wakiwa
wamepania kumpata, aligundua Genesis ni mtoto kutoka familia tofauti sana na
yake kiuchumi lakini hakuwa na majivuno na alikuwa muungwana.
Je, nini kitaendelea?
Simulizi : Kifo Siku Ya Harusi Yangu Sehemu Ya pili (2)Umeipenda? Dondosha coment kama unataka tuendelee na episode inayofuata
Comments
Post a Comment